Dar es Salaam. Chadema, ambayo pamoja na vyama vingine vitano vilisusia uchaguzi mdogo katika majimbo matatu, sasa ipo njiapanda kusimamisha wagombea katika majimbo ya Kinondoni na Siha.
Wakati bado hakijatangaza kubadili msimamo huo, uongozi wa ngazi ya Wilaya ya Kinondoni umeanza kutoa fomu kwa ajili ya mchakato wa kupata mgombea kwa maelezo kuwa umeruhusiwa na uongozi wa juu wa chama hicho kikuu cha upinzani.
Lakini uongozi huo wa juu umesema bado haujafanya uamuzi kuhusu kushiriki uchaguzi katika majimbo hayo uliopangwa kufanyika Februari 17 na msimamo huo unaweza kutolewa wakati wowote, Mwananchi imeambiwa.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Itifaki wa Chadema, John Mrema alisema jana kuwa wameunda kamati ndogo inayofanya utafiti kuhusu mchakato huo na kwamba uchukuaji fomu huo bado haujapewa baraka za ngazi za juu.
“Hatuna uamuzi wowote hadi sasa, ingawa ule wa awali wa kutoshiriki bado upo,” alisema Mrema.
“Lakini leo uamuzi utatoka. Bado tupo katika mjadala.”
Majimbo hayo mawili yanarudia uchaguzi baada ya waliokuwa wanayashikilia Maulid Mtulia (CUF, Kinondoni) na Dk Godwin Mollel (Chadema, Siha), kujiuzulu nafasi zao kwa nyakati tofauti na kuhamia CCM mwezi uliopita.
Mtulia alitangaza kujiuzulu ubunge Desemba 2 mwaka jana akisema hakushawishiwa na mtu yeyote, bali amebaini kuwa Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani yake na inafanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani uliahidi kuyatekeleza.
Wakati Mrema akisema bado wanajadili ushiriki wa Chadema, uongozi wa Wilaya ya Kinondoni umeshaanza mchakato wa kupata mgombea wa kumrithi Mtulia ambaye mwaka 2015 alisimamishwa na vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na makubaliano maalumu.
Uongozi huo umesema utasimamisha mgombea atakayepambana na Mtulia aliyepitishwa na CCM kuwania tena kiti hicho.
Mwenyekiti wa Chadema wa Kinondoni, Waziri Muhunzi aliiambia Mwananchi jana kuwa baada ya kutafakari kwa kina na kuona mwenendo katika uchaguzi uliopita wa marudio katika majimbo matatu, wameamua kuanza mchakato wa kumsimamisha mgombea.
“Chadema wilayani Kinondoni, ndio tulioamua kuuomba uongozi wa juu kusimamisha mgombea wa jimbo hili na tuna imani litarudi mikononi mwa Ukawa,” alisema.
“Ingawa jambo hili halikuwa rahisi, nawashukuru viongozi wa juu kwa kutuelewa na kuturuhusu.
“Ugumu ulikuwapo kutokana na msimamo wa viongozi wa juu kuhusu malalamiko yao waliyoyatoa huko nyuma kuhusu uchaguzi wa kata 43. Hata hivyo, uchaguzi wa majimbo matatu tumeona baadhi ya mambo yameanza kufanyiwa kazi ikiwamo polisi kutoingilia.”
Muhunzi alisema uchaguzi huo ni kipimo kwao cha kuangalia yale malalamiko dhidi ya wakuu wa wilaya kuingilia uchaguzi yatajitokeza tena kwa kuwa kwenye uchaguzi wa majimbo matatu uliofanyika hivi karibuni hayakujitokeza.
Alisema tayari wanachama 11 wamejitokeza kuomba nafasi ya kugombea ubunge wa jimbo hilo kati yao ni madiwani wanne.
“Mwisho wa kuchukua barua za kutangaza nia ya kuomba kugombea ni leo saa 10:00 jioni. Baada ya hapo kamati ya utendaji itakutana kwa ajili kutoa utaratibu wa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea jimbo hili.
“Thamani ya fomu ni Sh 250,000 ambazo watangaza nia hao watazichukua na kujaza kisha kuzirudisha kwa hatua nyingine zaidi,” alisema Muhunzi.
Muhunzi aliwataja wanachama waliojitokeza kutangaza nia kuwa ni Juma Uloleulole (diwani Kijitonyama), Agrey Nicolaus, Elisante Emmanuel, Moza Ally, Francis Nyerere, Rose Moshi (diwani viti maalumu), Ray Kimbita (diwani Hananasif) na Mustafa Muro (diwani Kinondoni). Boniface Obedi, Shabaan Moyo na David Assey.
Kuhusu Ukawa, Muhunzi alisema endapo CUF upande wa Maalim Seif Sharif Hamad ungemsimamisha mgombea, Chadema ingeheshimu uamuzi huo kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Kutokana na mgogoro unaondelea ndani ya CUF, tumesikia upande ule wa Profesa Ibrahim Lipumba unasimamisha mgombea, hivyo hatuwezi kuwaachia bora ingekuwa Maalim Seif,” alisema Mahunzi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema kura za maoni zinatarajiwa kufanyika leo na kwamba mchakato wa kukagua ujazaji wa fomu za kuomba ulikamilika jana.
Kwa upande wa Siha, kaimu mwenyekiti wa Chadema wa Kilimanjaro, Joseph Selasini alisema bado wanasubiri maelekezo ya Kamati Kuu ya chama hicho.
Hali kama hiyo ilijitokeza mkoani Singida ambako uongozi wa mkoa ulisimamisha mgombea jimbo la Singida Kaskazini, lakini viongozi wa taifa wakaagiza aliyepitishwa kugombea ajitoe kuheshimu msimamo wa chama hicho.